Sababu 5 muhimu kwa mama mjamzito kula viazi vitamu

Imesomwa mara 11063

Tutakuwa na makala za kuangalia mambo muhimu ya kuzingatia kwa mama wajawazito. Tutaangalia zaidi kuhusu lishe maana ndio kitu muhimu cha kupewa kipaumbele ili kuweza kumlinda mama na kumkuza mtoto. Hii ni sehemu ya kwanza katika mlolongo wa hizi makala.

Katika kipindi cha ujauzito, lishe ya mama ni kitu kinachotakiwa kupata kipaumbele zaidi. Chakula ndio kinachomjenga mtoto na kumpa mama virutubisho vinavyoboresha na kulinda mwili wake. Mama mjamzito anatakiwa kupata mlo kamili na bora ili kukidhi mahitaji yake na yale ya mtoto anayekua tumboni.

Lishe bora ni ile inayojumuisha makundi yote muhimu ya vyakula, lakini ni muhimu zaidi kama virutubisho hivi vitatokana na vyakula bora na vya asili kuliko vile vilivyoandaliwa kwa kutumia kemikali hatarishi. Katika makala yetu ya leo tunaangalia zaidi faida za viazi vitamu kwa mama mjamzito.

Faida za viazi vitamu

Viazi vitamu ni chanzo kizuri cha virutubisho, hasa kwa mama mjamzito. Baadhi ya virutubisho vinavyopatikana kwenye viazi ni kama :

1. Vitamin A

Vitamin A ni kirutubisho muhimu kwa kuboresha makuzi, macho na kuboresha kinga ya mwili. Hizi faida haziishii kwa mama peke yake, bali hata kwa mtoto anayekua tumbonni. Mama mjamzito anatakiwa apate miligramu 700 za Vitamin A kwa siku kwa kipindi chote cha ujauzito.

Kwa mtoto aliye tumboni, Vitamin A husaidia kwenye makuzi ya moyo, mapafu, figo, macho, mifupa na katika mfumo wa fahamu. Pia vitamin A huboresha kinga ya mwili na kuzuia maambukizi ya magonjwa kwa watoto.
Vilevile, baada ya Mama kujifungua vitamin A husaidia katika ukarabati wa tishu za mwili wake. Hivyo faida haziishii kipindi cha ujauzito pekee, bali kabla na hata baada ya ujauzito.

2. Vitamin B6

Vitamin B6 husaidia sana kumuondolea mama mjamzito homa za asubuhi (morning sickness) zinazoweza kumfanya apate kichefuchefu na kutapika. Pia vitamin B6 husaidia utengenezaji wa seli nyekundu za damu na kuboresha ubongo na mfumo wa fahamu wa mtoto.

3. Vitamin C

Vitamin C husaidia unyonyaji wa madini ya chuma ambayo ni muhimu sana kwa mama na afya mtoto. Kipindi cha ujauzito damu ya mama inatumika kwake na mtoto, hivyo lazima apate vyakula vinavyoweza kurahisisha kuongezeka kwa damu mwilini, kama viazi vitamu.

Vilevile, Vitamin C husaidia ukarabati wa tishu, kuponya majeraha, utengenezaji na ukuaji wa mifupa, kuboresha afya ya ngozi na pia husaidia mwili kupambana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Mama mjamzito anatakiwa apate miligramu 85 za Vitamin C na miligramu 27 za madini ya chuma kwa siku. Vitamin C ni muhimu sana kwa mtoto na upungufu wake husababisha kudumaa kiakili kwa mtoto mchanga.

4. Potassium

Potassium ni madini muhimu kwa mama mjamzito na pia anayenyonyesha kwenye kuboresha ufanyaji kazi wa seli za mwili na kuzuia maumivu ya miguu kwa mama mjamzito. Viazi vitamu vina kiwango cha kutosha cha madini ya potassium yanayoweza kukidhi mahitaji ya mama mjamzito.

5. Ufumwele (Fiber)

Ufumwele ni virutubisho vinavyopatikana zaidi kwenye mimea, ikiwemo viazi vitamu. Ufumwele husaidia kurekebisha matumbo na kulainisha choo. Kukosha choo ni tatizo linalowapata wamama wengi katika kipindi cha ujauzito. Ufumbuzi rahisi na usio na madhara ni kula vyakula vyenye ufumwele (nyuzinyuzi au fiber) ili kusaidia kwenye mmeng'enyo wa chakula na kumfanya mama apate choo kirahisi.

Mama mjamzito anatakiwa apate miligramu 25 za virutubisho vya nyuzi nyuzi kwa siku ili kuepuka kuvimbiwa (constipation). Hivyo ni vizuri kwa mama mjamzito kula vyakula asili ya matunda na mboga za majani.

Toa maoni yako