Mlo wa afya kwa mama mjamzito

Imesomwa mara 14409

Je mlo gani ni bora kwa mama mjamzito ?

Kipindi cha ujauzito ni kipindi ambacho mama mtarajiwa anatakiwa kupata mlo ulio kamili kwa muda sahihi na kiwango kinachotakiwa. Mlo kamili hutokana na vyakula mchanganyiko kutoka kwenye makundi yote muhimu ya vyakula. Kwenye makala yetu ya leo tunaangalia vyakula muhimu kwenye kujenga afya ya mama na mtoto anayekua tumboni.

Kupata mlo kamili huhakikisha mama anapata virutubisho vyote muhimu na kwenye kiwango sahihi kwa mahitaji yake na mtoto anayekua. Njia rahisi ya kuapta mlo sahihi ni kupata kiwango kinachotakiwa cha chakula kutoka katika kila kundi la vyakula. Umuhimu wa lishe bora ni kuufanya mwili kuongezeka uzito, kuzuia upungufu wa damu, kuboresha ukuaji na maendeleo ya mtoto aliyepo tumboni. Yafuatayo ni makundi tofauti ya virutubisho vya chakula yanayotakiwa kupewa kipaumbele kwenye mlo wa mama mjamzito.

1. Vyakula vya wanga ( kabohaidreti)

Wanga ni chanzo kikubwa cha nguvu mwilini. Vyakula vya wanga vimegawanyika katika makundi matatu wanga, sukari na ufumwele. Vyakula hivi hupatikana kwa wingi na kwa urahisi zaidi kwenye nafaka kama mahindi,mchele, mtama, ulezi na ngano. Vilevile, vyakula hivi hupatikana kwenye vyakula vya mizizi kama mihogo, viazi vikuu, magimbi na viazi vitamu.

Vyakula hivi huusaidia mwili wa mama kutengeneza mafuta, kuupa mwili joto na nguvu.

Ukosefu wa vyakula hivi huusababisha mwili kukosa mafuta, kudhoofika kwa nyama za mwili na kupungua uzito.

2. Vyakula vya wanyama (Dairy)

Vyakula vinavyotokana na wanyama kama mayai au maziwa vina virutubisho muhimu sana kwa mama mjamzito. Mama anapata vitamin, madini na virutubisho vingi sana kutoka kwenye maziwa. Kwenye maziwa yanapata madini ya Calcium ambayo husaidia ukuaji wa mifupa ya mtoto.

Vilevile kuna protini, vitamin D na phosphorus. Ieleweke kuwa mama mjamzito anahitaji protini asilimia 60 zaidi ya kiwango anachohitaji mama asiye mjamzito.

3. Jamii ya kunde

Vyakula hivi ni vyanzo vya protini, ufumwele na vitamin kwa wingi. Ni vyakula ambavyo havigharimu fedha nyingi na vinapatikana kwa wingi. Maharage yana kiwango kikubwa sana cha protini ambayo hutumika mwilini moja kwa moja bila kuleta madhara zaidi mwilini.

4. Mafuta

Vyakula vyenye mafuta ni kama vile alizeti, nazi, mawese, omega 3 na mbegu zinazotoa mafuta. Mafuta yakiongezwa kwenye chakula huboresha usharabu wa baadhi ya vitamin na huongeza kiasi cha nishati. Kuna baadhi ya samaki wana mafuta yenye uwepo wa virutubisho vya omega-3 ambavyo husaidia kuboresha ubongo, hasa wa mtoto anayekua. Virutubiosho hivi pia hupatikana kwenye mayai ya kuku wa kienyeji.

Mafuta haya humsaidia binadamu kua na uwezo mkubwa wa kufikiria na kutunza kumbukumbu. Pia mafuta husaidia mtoto kuzuia magonjwa kama autism, kisukari. Pia ni kinga nzuri kwa mama kwenye kuzuia kifafa cha mimba.

Mama mjamzito anatakiwa kupata gramu 250 za mafuta kila Siku kwa kipindi cha mwisho cha ujauzito. Hii itasaidia kujenga ubongo na mfumo wa fahamu wa mtoto.

Toa maoni yako