Vitu 10 muhimu jikoni kurahisisha maisha

Imesomwa mara 6492

Maisha ni mazuri pale unapoweza kufanya vitu vingi kwa ufasaha na kwa muda mchache. Siku hizi huna haja ya kuanza kuhangaika na mkaa uliolowa na mvua ili kuchemsha yai au kuanza kutengeneza mchicha, tumehamia kwenye gesi. Ni maendeleo ambayo kwa miaka 10 iliyopita wengi wetu walikuwa hawategemei kuyaona. Waswahili wanasema pole pole ili mradi unasogea.

Sasa, kupika ni sanaa, na fahamu kuwa mapishi ni yaleyale lakini matokeo ni tofauti kwa kila mmoja. Ni vizuri kama ukiwa na uwezo wa kuandaa vitu tofauti nyumbani ili upate kuwapa ladha nzuri ya vyakula na maisha wale uwapendao.

TIP : Wakati wa kuchagua vitu vya kutumia jikoni, nunua vitu ambavyo vinaweza kutumika kufanya kazi zaidi ya moja. Usinunue vitu na kurundika jikoni bila kuwa na matumizi maalumu. Lengo kubwa ni kufanya matumizi mazuri ya hela yako.

Leo ningependa tutupie jicho kwenye vitu muhimu vya kuhakikisha kuwa vipo jikoni ili kuweza kuwa na uhuru wa kuandaa vyakula tofauti nyumbani kwako. Je ni vitu gani unavifikiria muhimu kuwa navyo nyumbani ? Kabla hujanieleza, mie nina listi yangu hapa ya vitu muhimu jikoni :

Jokofu

Kama unahitaji kuwa na amani wakati wa kupika nyumbani kwako, ni muhimu sana kuwa na jokofu. Bila jokofu inawezakana maisha yako yakawa magumu sana. Hivyo ni vizuri kuwa na jokofu bora na linalodumu ili kuhakikisha unakuwa na amani nyumbani kwako.

 Oven

Kama unapenda kuandaa vyakula tofauti, oven ni kitu muhimu. Unaweza kuandaa vyakula toafuti, vitafunwa na vinginevyo kama ukiwa na oven inayofaa. Chagua oven nzuri inayodumu, weka nyumbani na uanze kuandaa mapishi unayotaka bila kikomo.

 Whisk

Wisk ni kifaa kinachotumika kukorogea mayai au mchanganyiko wa uji uji. Ni muhimu kutumia hii maana hufanya mchanganyiko wako kuwa na uwiano sawia, hasa kwenye kuchanganya vitu ambavyo ni vigumu kuchanganyika mfano mafuta na maji au mafuta na vinegar. Ila kama vyakula vyako unavyoandaa haviitaji kuchanganya changanya vitu, ni bora kuacha kununua maana hutokuwa na matumizi nayo muhimu.

Vipimo

Ili kuweza kujifunza kupika mapishi tofauti, ni muhimu kuwa na vipimo jikoni. Hii hukusaidia kuweza kuandaa kitu kutokana na maelekezo ya watu wengine, mfano mzuri ni kwenye kuandaa chakula cha kuoka. Kufuata mapishi kwa vipimo hupelekea matokeo mazuri zaidi. Fahamu kuwa kuna aina mbili za vikombe vya vipimo – vile vya vitu vikavu na vile vya maji maji. Ni vizuri ukiwa navyo vyote ili kuweza kuwa na uhuru wa kufanya unachotaka.

Microwave

Kama wewe ni mvivu kupika, usinunue microwave, jifunze kuandaa chakula vizuri kwanza kabla ya kununua hii. Ila mie nadhani microwave ni muhimu sana kukaa jikoni, maana ina manufaa mengi zaidi kuliko unavyodhani. Hata kama matumizi yake si mengi katika mapishi ya kila siku lakini bado ina umuhimu. Unaweza kuangalia matumizi muhimu ya microwave hapa (Bofya) ili kujua zaidi. Wengi wanasema Microwave ina madhara, lakini sijawahi kupata uthibitisho, hivyo natumia maana ni kitu kinachorahisisha sana maisha nyumbani.

Ubao wa kukatia

Ubao wa kukatia muhimu sana, lakini huna haya ya kununua wa bei ghali. Kumbuka kuwa ubao wa kukatia unatakiwa kufanya kazi ya kuzuia kuharibu vyombo au sink lako wakati wa kukaka vitu. Hivyo, nunua ule wa bei rahisi zaidi, maana kama unaweza kufanya kazi inayotakiwa huna haja ya kupoteza hela kwa kitu kikubwa zaidi.

Visu vikali 2 na cha kunolea

Visu ni kitu muhimu sana jikoni. Uwepo wa kisu hukuhakikishia kuweza kukata kitu cha aina yeyote ile nyumbani kwako – chukua visu viwili – kisu kidogo na kisu kikubwa. Ili kupata kisu bora, ni vizuri ukajaribu kushika kila mshikio wa kisu na kuchagua kile kinachoshikika vizuri mkononi. Ni muhimu kununua cha kunolea pia ili kuwa na visu vinavyokuwa na makali wakati wote. Visu vikali vinarahisisha maisha, vinakufanya unatumia muda mfupi na kupunguza ajali zinazoepukika. Ukitumia kisu butu unapoteza muda pasipo manufaa.

 Vifaa vya kukaangia

Ni ukweli kuwa katika vyakula vyako utahitaji kukaanga chakula hata mara moja. Ni muhimu kuwa na kikaango (Frying Pan), kikorogeo cha chuma chenye mshikio imara wa mbao au plastiki na chujio la bati lenye kuweza kuweka chakula kilichotoka kwenye mafuta moto. Hivi vitasaidia kufanya kazi kwa kuaanga samaki, nyama, chips na vingine vingi.

Miko ya mbao

Uwe unapika mboga, wali, ugali,  mchuzi au chakula cha aina yeyote, mwiko ni muhimu. Sababu tunatumia sufuria za bati, inashauriwa kutumia mwiko wa mbao sababu hauchubui sufuria. Hivyo, nunua mwiko wako, chagua mwiko wa wali au mboga (ina kama kishimo, au unafanana na upawa) na mwiko wa ugali (Uko bapa, mahsusi kwa kusonga ugali). Ukiwa na miiko miwili inatosha, huitaji zaidi.

Mifuko ya kuhifadhia chakula

Kuhifadhi chakula ni muhimu. Kuna vyakula vingine hutakiwa kuandaliwa na kuhifadhiwa kabla ya kuliwa baada ya muda mrefu. Kuna vyakula vingine huliwa na kubaki, hivyo ni vizuri kuhifadhi kwa matumizi ya baadae. Vyovyote itakavyokuwa, mifuko ya kuhifadhia masalia ua chakula ni muhimu kuwa nayo. Inapunguza kazi ya kuosha vyombo au kukupunguzia idadi ya vyombo unavyotumia kwa kuhifadhia kwenye jokofu.

Je wewe una vitu gani unavyodhani ni muhimu kuwa navyo jikoni kwako? Tudokeze, na upate kuongeza kwenye orodha hii. 

Toa maoni yakoAlphonce Mkangakoro
14:02, Thu 11 Dec 2014
Maoni yangu ni kwamba ainisha vifaa hivyo kwa lugha angalau ya kiswahili na ya kiingereza sanjari na matumizi kwa kila kifaa muhimu jikoni ili kusaidia pia wanafunzi wanaojiandaa na Mitihani ya cookery (wanaosoma FOOD AND NUTRITION).
Dadia Msindai
13:15, Fri 19 Dec 2014
@Alphonce. Nikiangalia kwenye hiyo habari naona kuna maelezo ya kila kitu kwenye majina ya kiingereza na kiswahili. Unaweza kufafanua kiasi ili nipate kuelewa jinsi ya kufikisha ujumbe huu kwa walengwa?

Tunashukuru kwa mchango wako. Tutaboresha jinsi ya kufikisha ujumbe kwenu. Endelea kuwa nasi kwenye tovuti yetu ya Misosi.