Je wajua matumizi haya ya Microwave?

Imesomwa mara 3892

Teknolojia inatuleta mambo mapya kila kukich. Kila kitu kinachogunduliwa huwa na uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja, lakini kujua matumizi ya vitu vingi lazima uwe mdadisi. Misosi Team inapenda kukurahisishia maisha kwa kukupa tips muhimu kwenye anga tofauti za maisha, hasa kwenye maswala ya nyumbani na mapishi. Leo tunaangalia orodha ya matumizi ya microwave yako, maana yako mengi, na haya ni baadhi tu ya yale tunayofahamu.

Microwave, ni kifaa kinachotumika nyumbani kutoa urahisi kwenye kupasha moto vyakula, haya ni matumizi mahsusi ya microwave. Microwave hufanya kazi kwa kutoa mionzi ya joto.  Kutokana na hili, unaweza kutumia microwave kwenye kazi mbalimbali kutokana na ubunifu na udadisi wako.

Jaribu vitu vyote, lakini usije kuweka kitu cha jamii ya CHUMA au BATI kwenye microwave, maana hii ni hatari na inaweza kusababisha matatizo makubwa kuliko kawaida.  Unaweza kuona madhara kwa kubofya video hapa 

Yafuatayo ni vitu vichache kati ya vingi unavyoweza kufanya nyumbani kwako na microwave:

 • Kupasha moto chakula
  Kama ilivyogusiwa mwanzo, haya ni matumizi mahususi ya Microwave.

 • Kuondoa bakteria
  Kutokana na kutoa mionzi ya joto, Microwave hutumika kama njia mojawapo ya kuua vijijudu (sterilizing) vitu mbali mbali (kasoro vyenye jamii ya chuma). Hii ni mahususi kwa sie tunaoosha vitu kwa maji yasiyo salama au kwa wale waandaao vyakula vya watoto wadogo na wanapenda kuwapa vyakula kwenye vifaa ambavyo ni safi na salama. Ni jambo la kuosha vyombo, unakausha kisha unaweka kwenye microwave na kuwasha kwa sekunde 30 hadi dakika 1.

  Unaweza pia kuondoa bakteria kwenye vifaa vya kusafishia vyombo mfano sponji ya kuoshea vyombo, taulo za kukaushia vyombo n.k.

  Ni njia nzuri sana ya kuhakikisha unaepukana na magonjwa kama typhoid na homa ya matumbo kwa wale wanaotumia maji yasiyo salama kwenye kuosha vyombo kabla ya kula.

 • Kupikia chakula
  Watu wengi walio waseja (single) na hawana muda mwingi wa kupika vyakula hutumia Microwave kama jiko kupika vyakula vyao.  Kutokana na ubunifu wako, unaweza kupika vyakula aina mbalimbali na vikatoka vizuri kama vimepikwa kwa jiko la kawaida - tofauti ni kuwa, kwenye microwave vinaiva haraka zaidi.

  Mfano mzuri ni kupika wali kwa muda wa chini ya dakika 10. Hii ni mahsusi kwa wale ambao ni waseja na wanangependa kula vyakula nyumbani bila ya kupitia hatua tofauti za kuanza kuandaa jiko na kuchungulia chakula kila dakika. 

 • Kulainisha Asali
  Je wewe unahifadhi asali nyumbani? Kama ulishawahi utafahamu kuwa asali ikikaa muda mrefu inatengeneza mabonge. Sasa ukitaka kulainisha hii asali unaweza kutumia microwave. Ni rahisi sana. Unaweka asali kwenye chombo kinachoweza kuingia kwenye microwave kisha unawasha microwave kwa muda wa sekunde 30 hadi dakika moja, baada ya hapo asali yako itakuwa imelainika.

 • Kuchemsha chai
  Je unataka kunywa chai kirahisi bila kuanza kupata shida ya kuwasha jiko la gas na kubandika surufia ua birika la maji? Basi jibu lako liko kwa microwave.  Weka kikombe cha maji, changanya majani ya chai, kahawa au maziwa, kisha washa microwave kwa muda  wa dakika moja. Unaweza kujiramba na chai yako.

 • Kupata maji mengi kwenye ndimu au limao
  Kule uswazi kwetu nilishazoea kuona wamama wakitaka kukamua ndimu au limao wanalipiga au kuliponda. Nilipouliza nikaambiwa inasaid kufanya litoe maji mengi. Si vibaya kufanya ndimu au limao kuwa na maji mengi, lakini tatizo ni kuwa ukiponda ndimu au limao linaongeza uchungu au uchachu zaidi, na linapoteza ladha. Jibu madhubuti nimekuja kulipata kwenye microwave. Weka ndimu au limao kwa sekunde 30 tu, kisha likate katikati, huwezi amini kiasi cha maji yatakayopatikana, na hutopata shida kukamua.

Je ulikuwa unafahamu mangapi kati ya haya? Kama una matumizi zaidi tafadhali usisite kuongeza hapa kwenye maoni. 

Toa maoni yako