Kisamvu cha nazi na maziwa mgando

Je uko tayari kujaribu vitu vipya ? Haya, kama kawaida wakati wa kujaribu mambo ukafika, nilisaka kila sehemu jinsi ya kuandaa chakula tofauti nikagonga mwamba, nikakumbuka kuwa sijawahi kupika kisamvu na sour cream. Na ndio nikafika huku. Matokeo yake si ya kusimuliwa, maana huwezi kuhisi harufu wala utamu hadi upate hii mboga mbele yako, na hapo itakuwa kujiramba hadi basi. Mie wakati wa kula nikachanganya hili samvu na mchuzi wa nyama ya ng’ombe, ndio mambo yakaita zaidi. Kama huifahamu sour cream au maziwa ya mgando, basi sour cream ni maziwa yaliyochechushwa kwa madhumuni ya kutumia kama kiungo cha chakula. Yako kama mtindi vile lakini usio na sukari wala vikorombezo vingine.

Mahitaji

 • Kisamvu (Angalia kinachowatosha)
 • Kitunguu
 • Nyanya chungu
 • Pilipili (Hii ya kuleta harufu nzuri, siyo lazima kama unakula na watoto wasiokula pilipili)
 • Kitunguu saumu 1
 • Mafuta ya kula kijiko 1 kikubwa cha mezani (Mie nimetumia olive oil)
 • Sour cream (Maziwa ya mgando)– vijiko 4 vikubwa
 • Chumvi – kijiko 1 cha chai
 • Nazi – kikombe 1 (Changanya tui zito na jepesi. Kama hutumii nazi unaweza kutumia karanga, ingawa ladha haitokuwa kama kwenye hiki chakula)

Wapi kwa kupata bidhaa?

Je wewe unauza hivi vitu kwenye biashara yako? Bofya hapa kutuma maelezo ya biashara yako hapa ili uweze kuwafikia walaji wako.

Maelekezo

Mapishi haya ya kisamvu nimeyapenda maana yalikuwa na ladha ya kipekee. Maziwa mgando au Sour cream ni maziwa yaliyochechushwa kwa madhumuni ya kutumia kama kiungo cha chakula, ni kama mtindi vile usio na sukari. Wakati mwengine nikiishiwa sour cream huwa natumia pia maziwa ya kawaida na huwa yanatoka vizuri, lakini wewe ni chaguo lako.

Kama hupendi maziwa unaweza kutumia karanga kwenye kuandaa kisamvu hiki na utapata matokeo mazuri pia ingawa ladha yake haiwezi kufikia hiki kisamvu hapa. Mie nilichanganya na mchuzi wa nyama kiasi ili kupata mchanganyiko mzuri zaidi wa mboga na mchuzi.

misosi-samvu-hiloooo

 • Andaa kisamvu – osha, kisha twanga vizuri kwenye kinu hadi kiwe laini. Kama una blender pia unaweza kukisaga kwenye blender, lakini njia nzuri zaidi ni kukitwanga.
 • Weka kisamvu kwenye sufuria, ongeza maji ya kutosha kisha bandika jikoni, funika vizuri na mfuniko. Acha kichemke vizuri kwa muda mrefu, maana kisamvu hakiivi mapema – mie nilikadiria kati ya dakika 45 hadi 50.
 • Wakati kisamvu kinachemka, andaa nazi, kitunguu saumu na kitunguu maji. Kamua tui la nazi, weka pembeni.
 • Menya kitunguu saumu na kitunguu maji. Kata kitunguu maji vipande vidogo. Saga kitunguu saumu vizuri. Hifadhi vizuri pembeni.
 • Ni vizuri pia kama ukichemsha nyanya chungu wakati kisamvu kinaiva. Chemsha kwa dakika 10 hadi 15 kisha menya ganda na uweke pembeni.
 • Kisamvu kikiwa tayari, epua na weka pembeni kisha bandika sufuria au kikaangio tofauti. Weka mafuta, kisha weka kitunguu saumu. Koroga kiasi, ongeza kitunguu maji. Koroga hadi vitunguu viwe laini na vianze kubadilika rangi. Weka pilipili ili ilete harufu nzuri. Ongeza na chumvi kisha koroga.
 • Weka kisamvu kwenye sufuria yenye vitunguu, changanya vizuri. Acha ichemke na vipate kuungana pamoja. Mwagia tui la nazi, koroga na usiache hadi lianze kuchemka.

Sheria ya tui la nazi ni kuwa lazima ukoroge hadi lianze kuchemka ndio uache, mara nyingi ukiacha bila kukoroga linakatika, hivyo kuwa makini.

 • Tui likianza kuchemka acha likae kama dakika 4 hadi 5 lipate kuungana na mboga vizuri kisha weka sour cream. Koroga vizuri sana. Ongeza nyanya chungu, koroga kiasi. Angalia zisipondeke maana zimeshaiva vizuri. Acha mboga ichemke hadi iive vizuri.
 • Baada ya muda mboga ikishaiva, toa na tenga ujirambe. Unaweza kula mboga hii na vyakula vingi – ugali, wali, n.k.

kisamvu-nazi

misosi-samvu-other

 


MAPISHI YAPENDWAYO

Biryani ya nyama
dakika 45
Walaji: 6

Ndizi utumbo za nazi
dakika 45
Walaji: 4

Tembele
dakika 10
Walaji: 4

Mishikaki ya kupaka
dakika 45
Walaji: 3

Toa maoni yakoJIRAMBE..

Tafuta sehemu ya kula karibu yako

MISOSI AKAUNTI YAKO
Huna akaunti? Bofya hapa kujisajili.