Njegere za nazi na maziwa

Njegere, mboga bora tunayokula mara kwa mara kwenye jamii yetu na yenye virutubisho vingi na kazi muhimu kujenga mwili. Je unapenda njegere? Basi hizi ni baadhi tu ya faida zake - kurekebisha kiwango cha lehemu (cholesterol) mbaya mwilini, kuimarisha mifupa, kuboresha mfumo wa kinga mwilini. Vilevile, ni mboga nzuri kuliwa na mtu anayetaka kupunguza uzito.

Mahitaji

 • Njegere ½ kilo
 • Maziwa mgando vijiko 2 vikubwa, au maziwa fresh ¼ kikombe
 • Nazi 1, vunja, kuna na tengeneza tui zito
 • Nyanya 2, menya kisha kata vipande, unaweza pia kusaga (Au pia unaweza kutumia nyanya ya kopo)
 • Karoti 2, menya kisha kata vipande vidogo
 • Kitunguu saumu kijiko 1 kidogo
 • Kitunguu maji 1, menya kisha kata vipande vidogo
 • Mafuta ya kula kjiko 1 kikubwa

Wapi kwa kupata bidhaa?

Je wewe unauza hivi vitu kwenye biashara yako? Bofya hapa kutuma maelezo ya biashara yako hapa ili uweze kuwafikia walaji wako.

Maelekezo

Mapishi haya ya njegere yana ladha zaidi kutokana na uwepo wa nazi na maziwa. Kama hutumii nazi unaweza kutumia karanga kama mbadala kwenye hii mboga, au unaweza tu kupika kwa maziwa na ikatosha. Maziwa yanaleta vionjo vitamu zaidi, na kuipa mboga hii utamu zaidi.misosi-njegere-2

 • Osha njegere kisha weka kwenye sufuria yenye maji. Bandika jikoni, acha hadi ziive vizuri na maji yakauke. Bandua na weka pembeni.
 • Bandika sufuria tofauti jikoni. Weka mafuta, acha yapate moto. Weka kitunguu saumu, koroga. Weka kitunguu maji. Acha kiive na kulainika, ila hakikisha hakiungui. Weka nyanya na chumvi. Koroga vizuri kisha funika acha hadi ziive.
 • Weka karoti, koroga vizuri. Weka njegere, kisha koroga pamoja ili zichanganyike vizuri na viungo vingine. Funika kwa takribani dakika 5 hadi 7.
 • Ongeza nazi, kisha koroga taratibu hadi tui lichemke vizuri ili lisikatike. Tui likishachemka kwa dakika 5, ongeza maziwa. Koroga taratibu hadi mboga ichemke tena.
 • Mie hupendelea kuponda njegere hadi uji wake utoke na mboga iwe na mchuzi mzito. Hivyo kama unapenda, unaweza kuponda pia, maana mchuzi unakuwa na ladha tamu zaidi ukiwa na uji mzito wa njegere.
 • Ukimaliza acha ichemke kwa dakika 3 hadi 5 kisha epua.
 • Unaweza kula mboga hii na wali, ugali, viazi, ndizi na vyakula vingine vingi. Jirambe  na ladha ya maisha.

misosi-njegere


Toa maoni yakoJIRAMBE..

Tafuta sehemu ya kula karibu yako

MISOSI AKAUNTI YAKO
Huna akaunti? Bofya hapa kujisajili.