Nyama yenye bilinganya na bamia

Hii ni mboga ya mchanganyiko wa nyama na mboga za majani. Napenda kuchanganya hivi maana mboga inakuwa na ladha nzuri na pia kuwa na virutubisho murua kwa pamoja. Ni mboga yenye virutubisho vingi mfano protini na nyuzinyuzi toka kwenye nyama na pia kwenye mboga za majani.

Mahitaji

Mahitaji ya jumla

 • Nyama ya ng’ombe ½ kilo
 • Bilinganya 1
 • Bamia 6
 • Nyanya 3 (Ukishamenya ponda vizuri ili iwe rojo laini, au tumia tomato paste)
 • Vitunguu 2
 • Pilipili hoho 2 (napenda zenye rangi tofauti ili kuleta rangi nzuri kwenye chakula)
 • Chumvi
 • Pilipili manga ya unga
 • Kitunguu saumu 1 (menya na kusaga) au cha unga kijiko 1 cha chai

Mahitaji maalum kwa ajili ya nyama

 • Limao au ndimu
 • Tangawizi, imenywe na kupondwa vizuri

Wapi kwa kupata bidhaa?

Je wewe unauza hivi vitu kwenye biashara yako? Bofya hapa kutuma maelezo ya biashara yako hapa ili uweze kuwafikia walaji wako.

Maelekezo

Tunapika chakula hiki kwa hatua mbili. 

1. Kuandaa nyama

 • Kata nyama kwenye vipande vidogo vinavyokufaa. Osha na kisha weka kwenye sufuria au chombo kikavu. Weka chumvi, changanya vizuri. Weka tangawizi. Koroga pamoja. Weka kitunguu saumu. Koroga pamoja. Acha nyama ikae kwa muda wa dakika 10 hadi 15 ili viungo viingie vizuri.
 • Bandika nyama jikoni. Usiongeze maji. Acha ichemke hadi maji yakauke. Ongeza maji, kama ujazo wa nusu lita, mie napenda nyama iwe laini wakati wa kula. Acha ichemke hadi maji yaanze kukauka, angalia kama imeiva. Ikiwa haijaiva ongeza maji na acha iive vizuri. Nyama ikiiva toa na hifadhi pembeni.

2. Kuandaa mboga za majani

 • Menya kisha kata kitunguu na karoti kwenye vipande vidogo unavyopendelea. Mie huwa napendelea vipande virefu vyembamba. Osha kisha kata pilipili hoho kwenye vipande vya wastani. Osha bamia kisha kata ncha, halafu kata kwenye vipande viwili au ukubwa unaopenda. Unaweza pia kupasua katikati, ni uamuzi wako.
 • Osha bilinganya vizuri. Kata kwenye vipande vidogo unavyopendelea. Kwa mapishi haya ni vizuri bilinganya liwe kwenye vipande vidogo ili lipate kuiva vizuri na haraka. Kukaa sana kwenye moto kunapunguza virutubisho vilivyomo kwenye chakula.
 • Weka bilinganya kwenye sufuria, ongeza maji kidogo sana. Ongeza chumvi. Kisha weka jikoni. Funika vizuri na acha bilinganya liive vizuri na maji yake.  Baada ya kuchemka vizuri toa na hifadhi pembeni.
 • Bandika sufuria au kikaango jikoni. Weka mafuta kwenye kikaangio. Subiri yapate moto kisha weka vitunguu saumu. Koroga koroga ili kisigandie kwenye sufuria. Weka pilipili manga, koroga kiasi.
 • Weka kitunguu maji. Koroga vizuri. Weka bamia, koroga kisha acha viive kwa pamoja. Takribani dakika 3 hadi 5.
 • Weka nyanya, koroga kiasi. Funika vizuri zipate kuiva. Subiria kwa dakika 5 hadi 7 kisha weka pilipili hoho, koroga mchanganyiko vizuri. Baada ya dakika moja weka karoti na endelea kukoroga. Acha viive kwa dakika 5 hadi 7.

Mie napenda mboga mboga zisiive sana ili virutubisho visipote. Kama unaona muda elekezi hautoshi, unaweza ukaweka kwa muda mrefu zaidi ili iwe laini zaidi.

 • Weka bilinganya kwenye mchanganyiko wa mboga mboga. Koroga pamoja kisha acha vikae kwenye moto kwa dakika 3 hadi 5.
 • Weka nyama na mchuzi wake kwenye sufuria yenye mboga za majani. Koroga kwa dakika chache kisha funika vizuri. Acha ichemke kwa dakika 5 hadi 7. Kisha epua na mboga iko tayari kuliwa.
 • Unaweza kula mboga hii na chakula chochote kile – wali, ugali, n.k
 • Jirambe na ladha ya maisha.

MAPISHI YAPENDWAYO

Meat loaf
dakika 60
Walaji: 4

Mapishi ya nundu
dakika 15
Walaji: 3

Kuku wa kuoka
dakika 120
Walaji: 5

Toa maoni yakoJIRAMBE..

Tafuta sehemu ya kula karibu yako

MISOSI AKAUNTI YAKO
Huna akaunti? Bofya hapa kujisajili.