Zege - Chips mayai zenye viungo na mboga majani

Unapenda chips? Kama ndio, basi hii ni aina ya chips itakayokupa ladha zaidi. Chips za mayai zenye viungo tofauti mie huniliwaza sana. Napenda viungo, hasa nikiandaa kwenye chakula kitamu kama hiki - fahari ya macho, ladha mdomoni na afya mwilini. Upewe nini tena maishani hapa?

Mahitaji

 • Viazi mbatata 4, vyenye ukubwa wa wastani
 • Pilipili hoho 2 (nimetumia zenye rangi tofauti)
 • Mayai 2
 • Chumvi
 • Kitunguu maji 1
 • Mafuta ya kula (Yanayotosha kukaangia chips)

Mahitaji ya ziada, si lazima kama hupendelei viungo kwenye chips. Mie huwa napenda harufu ya viungo kwenye chakula, hasa mayai.

 • Kitunguu saumu
 • Pilipili manga

Wapi kwa kupata bidhaa?

Je wewe unauza hivi vitu kwenye biashara yako? Bofya hapa kutuma maelezo ya biashara yako hapa ili uweze kuwafikia walaji wako.

Maelekezo

Nilikuwa na hamu ya kula zege – chips mayai. Ikabidi niandae hizi kwa hatua chache na rahisi. Kusema kweli ilikuwa tamu. Unaweza pia kuandaa kama hujawahi kwa kufuata hatua hizi chache.

 • Menya kisha kata viazi kwenye vipande vidogo vya chips. Hifadhi kwenye chombo chenye maji safi. Weka chumvi ili  iingie kwenye viazi.
 • Andaa kitunguu maji – menya kisha kata vipande vidogo. Menya kisha saga kitunguu saumu. Kata pilipili hoho kwenye vipande vidogo. Hifadhi pembeni.
 • Bandika kikaango jikoni. Weka mafuta ya kula, acha yapate moto vizuri. Hakikisha moto mkali ili viazi vipate kuiva vizuri, mafuta yasipokuwa ya moto sana viazi huiva vibaya. Mafuta yakipata moto, weka viazi. Kaanga hadi viive vizuri. Mie huwa napenda kuona vinaanda kubadilika rangi kiasi na kukauka, lakini visiungue. Kisha toa na weka pembeni.

Hakikisha unatumia mafuta ya kutosha. Ukiwa na mafuta kidogo utapata shida kuivisha viazi. Vinaweza visiive vizuri au vikaungua kutokana na mafuta kutokuwa ya kutosha. Hivyo ni muhimu uwe na mafuta ya kutosha.

 • Punguza moto kiasi. Bandika kikaangio jikoni, weka mafuta kiasi. Yakipata moto weka kitunguu maji. Koroga kiasi. Acha kiive hadi kianze kubadilika rangi. Weka pilipili hoho, koroga vizuri.
 • Pasua yai, vuruga vizuri. Kama unatumia viungo huu ndio wakati wa kuongeza - Weka kitunguu saumu, pilipili manga na chumvi kiasi. Koroga pamoja. Hifadhi pembeni.
 • Ongeza viazi kwenye kikaango chenye kitunguu na hoho kilicho jikoni, changanya vizuri. Acha dakika moja kisha mwagia mchanganyiko wa yai. Mimina vizuri ili uenee kwenye kikaango chote. Acha chips ziive vizuri upande mmoja.  Geuza ziive upande wa pili. Epua na weka pembeni.
 • Andaa kachumbari unayopendelea. Tenga chakula na jirambe kwa nafasi yako.

misosi-chips-mayai-main


MAPISHI YAPENDWAYO

Chocolate pancakes
dakika 15
Walaji: 6

Vitumbua vya mayai
dakika 10
Walaji: 6

Brown rice, maziwa na karoti
dakika 60
Walaji: 1

Toa maoni yakoJIRAMBE..

Tafuta sehemu ya kula karibu yako

MISOSI AKAUNTI YAKO
Huna akaunti? Bofya hapa kujisajili.